ZIARA YA RAIS WA SLOW FOOD – CARLO PETRINI NCHINI KENYA MACHI 28 – APRILI 2, 2012

Ziara yake nchini pia itajumuisha ziara katika jamii na bustani za shule zifuatazo:
Machi 29
Nairobi – Kiambu. Bustani ya jamii ya Wangige
Bustani iko katika eneo la Wangige, kata ya Kiambu na inahusisha wanachama 20 ambao wamejumuika katika kikundi Wangige Self help Group. Bustani hii ilianzishwa kwa lengo la kuhamasisha jamii juu ya masuala ya mazingira, kilimo endelevu kutokana na kuendelea kusahau kilimo cha hapo awali na kuegemea kilimo cha kisasa.
Machi 30
Gilgil, Nakuru – Fiwagoh Mission School (Mradi wa bustani ya shule) (120km kutoka Nairobi)
Shule hii iko katika kijiji cha Diatomite Kariandusi, Gilgil, kata ya Nakuru. Ni shule ya mseto ambayo inahudumia watoto wa mitaani na watoto waliochwa yatima kutokana na janga la ukimwi.
Njoro, Nakuru – Chuo Kikuu cha Egerton (183km kutoka Nairobi)
Egerton ni chuo kikuu cha kilimo nchini lakini kimepanuliwa kujumuisha maeneo mengine ya utafiti na mafundisho kama vile: Maliasili, Sayansi , Elimu, Sayansi ya kompyuta, Sayansi ya matibabu, Uhandisi na masomo ya biashara. Katika Chuo Kikuu, Carlo Petrini atatoa hotuba kwa wanafunzi na maprofesa.
Machi 31
Njoro – Presidia ya Malenge ya Lare
Kitengo cha Lare kiko kwenye kingo za mashariki za msitu wa Mau, msitu ulio mkubwa zaidi katika Afrika Mashariki, na ni sehemu ya nyanda za juu kavu ya Bonde la Ufa, eneo ambalo limekumbwa na mabadiliko ya mtindo wa mvua hivi majuzi, na kuleta wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wa chakula. Zao moja ambalo limependekezwa kwa kustahimili madhara ya mabadiliko hayo ya hali ya anga ni lenge ambalo ni zao la jadi, na linalokuzwa katika sehemu hii.
Molo – Bustani la shule la Michinda
Bustani ya shule ya msingi ya Michinda, iko katika mji wa Elburgon, Kata ya Nakuru, ilianzishwa mwaka 2005 kwa msaada wa NECOFA (Network For Ecofarming in Africa), Slow Food Foundation for Biodiversity na Slow Food Central Rift Convivium. Bustani hii hulimwa na wanafunzi 50, shule ikiwa na jumla ya wanafunzi 400.
Aprili 1
Nakuru – Kitale, bustani ya familia ya Namgoi (225km kutoka Nairobi)
Bustani hii inahusisha Bwa. Wafula, mke wake na watoto wao sita ambao wana umri kati ya miaka miwili hadi kumi na saba. walinunua kipande cha ardhi ekari moja katika mwaka 2005, ambapo walianza mradi wa bustani kwa lengo la kukuza chakula safi na cha kutosha *familia. Matumaini yao ya baadaye yalikuwa kulifanya lile bustani kuwa kituo cha mafunzo kwa jamii nzima.
Aprili 2
Kitale – Kapenguria – Bustani ya shule ya Galip Litey
Inapatikana katika wilaya ya Kapenguria, iliyo  katika Kata ya Pokot Magharibi, wanafunzi 50 hushiriki katika bustani la Galip Litey.
Pokot Magharibi, Kenya – Presidium ya maziwa lala yenye jivu ya wapokot
Presidium hii inapatikana katika wilaya ya Pokot magharibi nchini Kenya. Kitamaduni jamii ya wapokot katika vijiji vya Tarsoi, Tartur, Lition na Chaunet wamekuwa wakitengeneza maziwa lala ya kipekee wakitumia maziwa ya ng’ombe (mchanganyiko kati ya mifugo wa kiasili na zebù) au mbuzi, ambayo hutiwa jivu kutoka kwa mti uitwao Kromwo.

Dhamira ya Slow Food Barani Afrika
Upatikanaji wa chakula na lishe ya kutosha ni matatizo yanayoathiri idadi ya watu wanaozidi kuongezeka katika nchi nyingi duniani. Kwa sasa kuna idadi ya watu bilioni 7 duniani, na mahitaji ya chakula yanaendelea kuongezeka jinsi idadi ya watu inavyozidi. Kulingana na FAO, chakula kinachozalishwa katika dunia kinaweza kulisha watu bilioni 11. Hata hivyo, zaidi ya watu bilioni moja bado wanaathiriwa na njaa sugu, wakati bilioni 1.5 ya watu wazima wana uzito uliopindukia. Shinikizo la rasilimali za dunia linapoendelea kuzidi, inakadiriwa kuwa 40% ya chakula kinachozalishwa kila siku hutupwa dunia kote. Hii ni dalili ya mfumo mbaya na usio na usawa wa uzalishaji wa chakula na mara nyingi ni maskini ambao hulipa bei iliyo ya juu zaidi duniani. Bara la Afrika huadhiriwa sana na hali hii, kutokana na hali ya uhaba wa chakula, kiwango cha juu cha matumizi ya rasilimali asili na uharibifu wa chakula kutokana na ukosefu wa miundomsingi. Kupitia kwa mradi wa bustani 1000 katika Afrika; kampeni dhidi ya unyakuzi wa ardhi, Presidia na masoko ya wakulima, Slow Food inasaidia jamii za Afrika ambazo zinapigania uhuru kutokana na maafa ya njaa na haki ya chakula. Mara nyingi, kujitolea kwa Slow Food katika miradi hii ina maana sio tu kuboresha hali ya maisha, lakini pia kuhakikisha kuwa jamii zaweza kuendelea na maisha.

Bustani elfu katika Afrika.

Ikilinganishwa na utata na uzito wa matatizo yanayolikabili bara la Afrika, kuanzisha bustani yaweza kuonekana kama ishara isiyokuwa na umuhimu. Lakini kama bustani elfu zaweza kuanzishwa katika takriban nchi ishirini na tano, na kama mitandao ya wakulima, wataalamu wa kilimo, wanafunzi na wapishi waweza kujitokeza katika kila mojawapo ya bustani, basi mradi huu waweza kutuelekeza katika siku endelevu zijazo, zitakazoambatana na mahitaji ya jamii. Hizi si siku ambazo zimeundwa na taasisi kubwa za kifedha za kimataifa ambazo simekuwa zikihamasisha mazao ya kuuza nje na mifumo ya kilimo yenye kuzingatia matumizi makubwa ya mbolea za kemikali. Wala sio siku zijazo zilizotabiriwa na wawekezaji wa kigeni, ambao hunyakua vipande vikubwa vya ardhi vilivyo na rotuba kwa bei ya chini ili kukuza mazao kwa manufaa ya nchi zao.

Hiki ndicho kiini cha uzinduzi wa mradi wa bustani elfu barani Africa mnamo mwaka 2011. Bustani zinazosimamiwa na waafrika; zilizoundwa kulingana na mahitaji yao, na zitakazo kuwa tayari wakati wa Terra Madre na Salone del gusto 2012. Mnamo mwaka wa 2011, waratibu wa kitaifa walikutana katika mikutano mbalimbali ili kuamua kitakachopandwa na ukulima unaofaa.
Waliweza kuamua suluhu tofauti kulingana na mazingira ya kila nchi, iwe oasisi ya Morocco, ardhi kame nchini Mali, nyanda za juu za Kenya au misitu ya Uganda. Hazitakuwa tu bustani za kawaida. Jamii zitazalisha mbegu zao, kuzingatia mazao ya kiasili (mboga, kunde, matunda na mitishamba ya upishi na dawa) na kutumia njia za asili za kutengeza mbolea, kupambana na wadudu na magugu. Mradi huu utahusisha vijana, lakini utaegemea msingi wa hekima ya wazee. Katika madarasa haya yasiyo na ukuta, chakula cha asili kitafunzwa na kuhamasishwa, na ubusara utasambazwa. Mradi unahusisha nchi 25 barani Afrika.

Kwa maelezo zaidi, tafadhali tembelea tovuti ya Slow Food Foundation for Biodiversity: www.slowfoodfoundation.org

Kuna uwezekano wa vyombo vya habari kushiriki katika baadhi ya ziara kwa jamii na bustani za shule.

Kwa ombi la mahojiano au maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:
Paola Nano – Slow Food International Press Director
[email protected]
Simu Italia +39 329 8321285
Simu Kenya +254707693824 (kutoka Machi 25)

Maelezo kwa Mhariri

Slow Food ni shirika la ngazi ya chini na la kimataifa ambalo hufikiria dunia ambayo watu wote wanaweza kupata na kufurahia chakula ambacho ni kizuri kwao, kizuri kwa wanaokikuza na kizuri kwa dunia. Ni Shirika lisilo la kiserikali linalosaidiwa na wanachama. Slow Food ilianzishwa mwaka 1989 ili kukabiliana na kupambana na chakula cha Fast Food na maisha ya haraka, kupotea kwa tamaduni za chakula na kuelimisha watu wawe na ufahamu wa chakula wanachokula, kinapotoka, ladha yake na jinsi chaguo letu la chakula linavyoathiri wengine duniani. Slow Food inaamini kwamba kila mtu ana haki ya furaha ya chakula bora na kwa sababu hiyo jukumu la kulinda urithi wa chakula, mila na tamaduni zinazowezesha kupatikana kwa furaha hii.

Slow Food ina wanachama zaidi ya 100,000 wiliojiunga katika Konvivia 1500 – vikundi vyetu vya mitaani – duniani kote, vile vile mtandao wa jamii 2000 za vyakula, zilizounganishwa katika mtandao wa Terra Madre, ambao hushirikisha wakulima wadogo na uzalishaji endelevu wa chakula bora. Shukrani kwa miradi na shughuli zake. Mtandao huu unahusisha mamilioni ya watu katika nchi 150.

Mtandao wa Terra Madre ulizinduliwa mnamo mwaka wa 2004 ili kuwapa sauti wakulima wadogo, wafugaji, wavuvi na mafundi wa chakula duniani ambao mbinu zao kuzalisha chakula, hulinda mazingira na jamii na pia kuwafanya watambulike. Mtandao huu huwaleta pamoja wasomi, wapishi, walaji na makundi ya vijana ili waweze kujiunga pamoja kwa minajili ya kuuboresha mfumo wa chakula. Jamii zinazokuza chakula huja pamoja kila baada ya miaka miwili katika tukio la kimataifa linalofanyika mjini Torino, Italia, ingawa mikutano ya kitaifa na kikanda huandaliwa mara kwa mara duniani kote.

Carlo Petrini (S. 1949) ni mwandishi, mwanzilishi na rais wa shirika la Slow Food. Anaishi katika mji mdogo wa Bra katika mkoa wa Piedmont, kaskazini mwa Italia. Tangu miaka ya 1970s, nakala zake zimechapishwa katika aina mbalimbali ya magazeti. Aidha, amechapisha vitabu kadhaa kuhusu gastronomia, au maendeleo endelevu na uzalishaji wa chakula ulio bora.

  • Did you learn something new from this page?
  • yesno